Fibroids Ni Kitu Gani? Ni Nini Tiba Ya Fibroids?
Fibroids ni uvimbe wa misuli laini wenye mizizi ya kuiunganisha unaoota na kukua kwenye uterus. Majina mengine ya uvimbe huu ni uterine fibroids, myomas, au fibromyomas. Fibroids ni aina ya uvimbe unaoonekana kwa wingi zaidi katika mfumo wa uzazi wa mwanamke. Fibroids ni uvimbe ambao mara nyingi (asilimia 99) hauna madhara kiafya na wala kuhusiana na ugonjwa wa kansa.
Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 20 hadi 50 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa, miaka 30 hadi 50, wana fibroids ingawa wengi wao hawahangaiki kuchukua vipimo vya fibroids. Uvimbe wa fibroids unakuwa na ukubwa tofauti tofauti, unaweza kuwa mdogo kama haragwe au kufikia ukubwa wa tikiti maji.
Chanzo Cha Fibroids
Sababu hasa za kuota kwa fibroids katika viungo vya uzazi vya mwanamke bado hazieleweki vizuri ingawa inaamika kwamba kila uvimbe wa fibroid unatokana na seli ya musuli wa uterus ambayo imeamua kuwa na tabia ya tofauti na nyingine na ikaanza kukua kwa haraka ikichangiwa na uwepo wa homoni ya estrogen.
Wanawake wanaokaribia kufikia ukomo wa kupata siku zao za mwezi wanaonekana kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata fibroids kwa sababu ya kuwa wameishi na homoni ya estrogen kwa muda mrefu zaidi. Wanawake wenye asili ya mchanganyiko wa wamarekani na waafrika (wamarekani weusi) nao wanaonekana kupatwa na fibroids zaidi ya wanawake wengine ingawa sababu bado haijajulikana.
Utafiti umeonyesha pia kuwa idadi ya wanawake wanaopatwa na fibroids katika kundi la wanawake ambao wamezaa watoto angalau wawili wakiwa hai huwa ni nusu ukilinganisha na wale ambao hawajazaa hata mara moja. Hapa haieleweki kama kuzaa kulizuia wanawake hawa wasipate fibroids au fibroids ndizo zilizozuia wanawake wa kundi la pili wasizae. Utafiti kuhusu hilli bado unaendelea.
Dalili Za Fibroids
Akina mama wengine wenye uvimbe wa fibroids huwa hawaoni dalili zo zote zile (wengi hawajui kama wana fibroids) au kuona dalili kidogo na kwa wengine dalili hizi hujitokeza sana na kuwasumbua hadi kufikia kutafuta tiba. Baadhi ya dalili za fibroids ni:
– Kutokwa na damu kwa wingi wakati wa siku au kutokwa na damu kwa muda mrefu
– Kutokawa na damu kusiko kwa kawaida katikati ya siku za mwezi
– Mauvimu ya nyonga (uvimbe kugandamiza kwenye viungo vya nyonga)
– Kupata haja ndogo mara kwa mara
– Maumivu ya mgongo
– Maumivu wakati wa tendo la ndoa
– Upungufu wa damu kwa sababu ya kutokwa na damu kwa wingi wakati wa siku
– Maumivu ya kichwa
– Maumivu kwenye miguu
– Kuvimba sehemu ya chini ya tumbo (Fibroids kubwa)
– Uzazi wa shida
– Mimba za shida
– Kutopata mimba
– Kutoka kwa mimba mara kwa mara
Aina Ya Fibroids
Kuna aina nne za Fibroids
Intramural: Fibroids aina hii hukua kwenye kuta za uterus. Hii ndiyo aina ya fibroids inayowapata wanawake wengi.
Subserosal fibroids: Fibroids aina hii hukua nje ya kuta za uterus na huweza kuwa na shina. Subserosal fibroids huweza kukua na kuwa kubwa sana.
Submucosal fibroids: Fibrioids aina hii huota na kukua kwenye misuli chini ya ngozi laini ya kuta za uterus.
Cervical fibroids: Fibroids aina hii hujenga kwenye shingo ya tumbo la uzazi (Cervix).
Tiba Ya Fibroids
Kama mwanamke hapati usumbufu wa namna yo yote katika shughuli zake za kawaida, anaweza asipewe tiba ya aina yo yote hata kama imegundulika kuwa ana uvimbe wa fibroid kwa sababu mwanamke anapokaribia kukoma hedhi fibroids hunyauka zenyewe na mara nyingine kutoweka kabisa.
Endapo tiba imekuwa ni ya lazima, anaweza kupewa dawa au kufanyiwa upasuaji kutokana na hali iliyopo.
Comments
Post a Comment