Wizara ya Elimu yatoa muongozo Vyuo Vikuu
Mkuu wa kitengo Cha Uratib wa Elimu ya Juu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Bi Aida Juma Maoulid amewataka Wakuu wa Vyuo nchini kuhakikisha Wanafunzi wanapata Elimu ya kutosha juu ya kujikinga na Covid 19.
Ameyasema hayo wakati alipofanya ziara katika Vyuo Vikuu mbalimbali vya Unguja kuangalia utaratibu wa ufundishaji katika kipindi hiki Cha maradhi ya Corona.
Amesema ipo haja kwa Vyuo kutoa Elimu kwa kutumia vipeperushi vyenye miongozo ya kujikinga na korona ili kuendelea kuondosha kabisa maradhi hayo nchini.
Nao Wakuu wa Vyuo wamesema bado jitihada ya kuelimisha Wanafunzi inahitajika hasa katika suala la uvaaji wa barakoa wanapokuwa katika mazingira ya Chuo na hata sehemu nyengine ili kuhakikisha maradhi hayo hayawapati.
Aidha wamesema katika Vyuo vyao wanaandaa kamati maalum za Wanafunzi ili kusaidia kuhamasishana juu ya kujikinga na maradhi hayo.
Wamesema kutokana na wingi wa Wanafunzi wameandaa utaratibu maalum wa usomeshaji ikiwemo kutumia kumbi kubwa za vyuo na kusoma kwa kutumia mtandaoni.
Kwa upande wao Wanafunzi wamepongeza uongozi wa Vyuo vyao kwa kuandaa mazingira ya kuridhisha katika mapambano ya maradhi ya Corona kwa kueka maji ya kunawia mikono ,vitakasa mikono na mashine za kupimia joto ,Jambo ambalo litawasababishia wao kusoma bila ya hofu ya kuambukizana.
Bi Aida amefanya ziara katika Skuli ya biashara Chwaka ,Skuli ya kilimo kizimbani,Chuo Cha Utawala wa umma (IPA),Chuo kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kampasi ya Tunguu na Chuo kikuu cha Zanzibar (ZU) iliyopo kibele Unguja.
Comments
Post a Comment