CHINA BADO INAHITAJI USHIRIKIANO WA KIELIMU NA KIUTAMADUNI NA ZANZIBAR
USHIRIKIANO katika
Sekta ya Elimu na Utamaduni kati ya China na Zanzibar umeelezwa kuwa umesaidia
sana katika kuendeleza urafiki baina ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Balozi mdogo wa
China aliepo Zanzibar Xie Xiao Wu alieleza hayo alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari katika Ubalozi wao uliopo Mazizini ikiwa
ni maadhimisho ya siku ya Walimu Nchini China.
Alisema utamaduni wa
China na Tanzania unafanana na wananchi wa nchi hizo mbili wamekuwa
wakishirikiana katika masuala mbali mbali ikiwemo biashara na makampuni ya
China kuaminika katika kujenga Ofisi za Serikali na watu binafsi.
Balozi Xie
alisisitiza kuwa China itaendelea kuisaidia Tanzania katika harakati zake za kiuchumi na hivi sasa
wanasimamia ujenzi wa viwanja viwili vya michezo Mao tse tung na
wanatarajia kujenga bandari mpya katika eneo la Mpigaduri Mjini Zanzibar.
Aliwapongeza vijna wa
Zanzibar kwa kuwa na mwamko wa kujifunza lugha ya kichina katika Chuo Kikuu cha
Taifa Zanzibar na Chuo cha Uandishi wa Habari na ameeleza matumaini yake
kuwa katika miaka michache ijayo vijana wengi watakuwa na uwezo wa kuitumia
lugha hiyo na kupanua wigo wa biashara kati ya China na Tanzania.
Kwa upande wake Mkuu
wa Chuo cha Uandishi wa Habari Zanzibar Chande Omar Omar aliishukuru
Jamhuri ya Watu wa China kwa msaada wa kuleta walimu kufundisha lugha hiyo
katika chuo hicho na mafanikio yameanza kuonekana kwani baadhi ya vijana
wanauwezo wa kusoma na kuzungumza lugha hiyo.
Alisema hivi sasa
zaidi ya wanafunzi 30 kutoka chuo cha Undishi wa Habari wamepata nafasi
ya masomo ya nchini China baada ya kufanya vizuri mitihani ya lugha ya
kichina chuoni hapo.
Aliongeza kuwa mbali
na wanafunzi hao, wanafunzi wengine tisa wa Chuo hicho wanatarajiwa kuondoka
hivi karibuni kuelekea nchini China kwa mafunzo zaidi ya lugha na fani ya
uandishi wa habari na watakaporejea watakuwa walimu wa wenzao katika vyuo mbali
mbali vya Zanzibar .
Comments
Post a Comment