NA: ALI MOHAMMED ALI

 AMEANDIKA KATIKA UKUTA WAKE WA MTANDAO WA KIJAMII FACEBOOK: ALI MOH'D
       
KIFO CHENGINE CHA KUSIKITISHA KILICHOSABABISHWA NA WATU WASIOJULIKANA ZANZIBAR.
Kwa masikitiko makubwa sana nimepokea taarifa za masikitiko makubwa kutoka kwa ndugu yangu rafiki yangu Hashim Shawej, juu ya msiba wa rafiki yetu Abdalla Juma. (Allah Amrehemu, amsamehe madhambi yake na amuingize katika jana).
Marehemu Abdalla Juma Slim ni mfanyakazi na nimpishi mahiri wa vyakula vya kimataifa (International Cuisine), kwa kazi yake hiyo usiku wa juzi tarehe 20/04/2017 alikuwa akitokea kazini mji mkongwe (Stone Town), alishuka gari ya kazini kwa Amani - Mabata ili apenye njia za ndani kuelekea nyumbani kwake Magomeni kwa mtumwa jeni, ndipo kikundi cha watu asio wajua wakamvamia kutaka kumkaba na kumuibia.
Kwa kuwa aliwapa shida katika kutimiza azma yao hio, wakaamua kumnadia mwizi ndipo watu wa mtaani wa eneo hilo la Kwa Mabata wakamvamia kwa kumpiga vibaya sana na kumsababishia majeraha makubwa pamoja na kupoteza damu nyingi sana, alijitahidi kujitetea kwamba yeye si mwizi bali waliomnadia mwizi wao ndio wizi, lakini hakuna aliyemsikiliza, hivyo Marehemu Abdalla akapoteza fahamu na waliompiga wote wakakimbia.
Wasamaria wema wakamuokota wakampeleka kituo cha polisi kwa ajili ya kupata PF3 kisha Hospitali ya Mnazi mmoja kwa ajili ya matibabu, ambapo Abdalla leo hii amepoteza uhai wake, Marehemu Abdallah hakuwahi kuiba hata siku moja, alikuwa ni kijana anayejishughulisha ili kupata rizki ya jasho lake.
Kwa sisi watu wanyonge serikali haina mpango wa kutuekea mazingira salama ya kulinda uhai wa wafanyakazi na nalazimika kusema sisi wafanyakazi wa chini hatuna thamani kwa serikali yetu hasa hasa sisi tunaofanya sekta binafsi ambao mara nyingi tunafanya kazi hadi usiku.
Serikali inatumbua kwamba kuna raia wanaolitumikia taifa hili usiku na mchana, serikali iko makini kukamua kodi za raia hawa, serikali iko tayari kuwashitaki na kuwachukulia hatua raia hawa pindipo wakikwepa kodi za jasho lao (P.A.Y.E), lakini serikali haiko tayari kunusuru maisha ya akina Abdalla Juma.
Wahalifu wamo mitaani wamezagaa, vigenge vyao vinaonekana na vinajulikana, tuna jeshi la kutosha kuweza kuwadhibiti hawa wahalifu ukizingatia na udogo wa nchi yetu, tuna vikosi vinavika makazini bila ya kuwa na kazi za msingi, vinaishia chini ya miti makambini kusubiria muda wao umalizike warudi wajumbani wakati huku wahalifu wakijipa uhalali wa kufanya uhalifu muda na wakati wanaojisikia.
Inasikitisha kuona Abdallah Juma aliyemzika babake hivi karibuni na kumuachia ulezi wa ndugu zake huku yeye mwenyewe akiwa na Mke na Watoto wa kuwalea na yeye anafanyiwa ukatili kama huu.
Naandika hapa kwa wino wa machozi nikitaraji wenye dhamana watalisikia hili, kwa kuwa matukio kama haya yanatukuta sana sisi watu wa chini, binafsi nina historia nyingi za matukio kama haya kwa kuwa kazi ninayoifanya inaniwajibikia yanipitie matukio kama haya.
Abdalla Juma hakuwa mwizi na hakuwahi kufikiria kuwa mwizi, bali Abdalla Juma alikuwa ni mtu mwema mwenye sifa za watenda wema.
Abdalla Juma umetangulia, na sisi tunafatia, tunakuombea Allah akusamehe makosa yako, ageuze makosa yako kuwa mema na mema yako yazidi uzito wa kukuezesha kuishi vyema katika makazi ya kaburini na hatimae uingie katika pepo na sisi Allah atupe khatima njema - Amiin
Inna lillahi wainnaa ilayhi raajiun.
Pichani ndiye Marehemu Abdalla Juma wakati wa uhai wake, atazikwa leo adhuhuri huko kijijini kwao Makunduchi.

Comments

michezo

MCHEZO WA KIRAFIIKI WASIMAMISHA VISIWA VYA ZANZIBAR KWA MASAA.

KUELEKEA MICHUANO YA KOMBE LA MAPINDUZI WAFAHAMU MABINGWA WA KOMBE HILO

Burudani ya mashindano ya Elimu bila malipo JKU na Makunduchi balaa.

TAARIFA ZA KURITADI KWA IDDI THABIT ( IT ) ZA KANUSHWA NA MWENYEWE

DABI YA JANG'OMBE TAIFA HOI,WALIMWA KADI NYEKUNDU